Taasisi ya Gusii Institute of Technology (GIT) iliyoko mjini Kisii imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia rabsha zinazotekelezwa kila mara na wanafunzi wa Taasisi hiyo.
Hii ni baada ya wanafunzi hao kuzua rabsha tena hapo siku ya Jumatano kufuatia kuuwawa kwa wanafunzi wenzao kwenye ajali iliyosababishwa katika lango la Taasisi hiyo wiki jana.
Akizungumza na Waandishi wa Habari siku ya Alhamisi jioni katika mji wa Kisii, Naibu Kamishna wa Polisi katika Kaunti ya Kisii Phillip Soi alisema kuwa waliamua kuifunga Taasisi hiyo kwanzia siku ya Alhamisi
Afisa huyo alisema kuwa uamuzi huo uliafikiwa baada ya miili ya wanafunzi wa Taasisi hiyo waliopoteza maisha kwenye ajali wiki jana kutolewa katika chumba cha kuhifadhi maiti na kusafirishwa nyumbani mwao huku wakihofia kuwa huenda wanafunzi hao wakazua rabsha.
“Yeyote atakayejaribu kuleta fujo siku ya Ijumaa wakati wale waliopoteza maisha yao wanazikwa atakabiliwa vilivyo kama mhalifu wala si kama mwanafunzi maana wanafunzi tumewaruhusu kwenda nyumbani,” alihoji afisa Soi.
“Mipango ya kufungua Taasisi hiyo itafanyika baadaye na wale wa kuenda mazishi wawe na utulivu na nawasihi wasijaribu kuleta vurugu hatua kali itachukuliwa dhidi ya yeyote atakayefanya hivyo,” aliongezea Soi.
Wakati uo huo, miili ya wanafunzi waliopoteza maisha yao ilisafirishwa hadi ndani ya uwanja wa Taasisi hiyo kabla ya kupelekwa makwao huku Maafisa wa usalama wakishika doria kwa hali ya juu.
Wanafunzi wa Taasisi hiyo wanapashwa kuwa watulivu na watatangaziwa tarehe rasmi ya kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.