Wazazi wanao waficha na kuwatetea watoto wao wahalifu wametahadharishwa kuwa watoto hao wakati mmoja watawahangaisha maishani mwao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Joseph Thuo ambaye ni Naibu wa Chifu wa Kata Ndogo ya Baraka katika Kaunti Ndogo ya Subukia alisema baadhi ya wazazi wanajua vyema kuwa wanao wanashiriki vitendo vya uhalifu, lakini wanakosa kuwaripoti kwa Maafisa wa usalama ili hatua mwafaka zichukuliwe dhidi yao.

Akizungumza siku ya Jumanne kwenye kikao kimoja cha wazazi katika eneo hilo, Naibu wa Chifu huyo alisema, “Baadhi ya wazazi wamekuwa kizuizi cha kukabiliana na utovu wa usalama vijijini kwani huwatetea wanao ambao wanajihusisha na uhalifu. Nawahakikishia wazazi kama hao kuwa baadae watoto hao watawadhuru kupitia vitendo vyao vya uhalifu.”

Naibu Chifu Thuo alikuwa akirejelea kisa cha juma lililopita ambapo jamaa mmoja aliwashambulia wazazi wake katika kitongoji cha Milimani na kukamatwa. Cha kushangaza kilikuwa ni kutetewa vikali kwa wazazi wa jamaa huyo ili aachiliwe huru na Maafisa wa Polisi katika kambi ya Kwa Mahinda waliomtia mbaroni.

Aidha inasemekana kuwa kijana huyo anayefahamika kama Muiruri aliye na miaka 30 ni mshukiwa wa ubakaji  na aliachiliwa na Mahakama baada ya wazazi wake kumtolea dhamana.

“Wazazi wana jukumu la kuwalea watoto wao kwa maadili yafaayo na kwa misingi ya Ukristo ili mwishoe waone wanao wamefanikiwa maishani mwao,” alisema Thuo.

Naibu Chifu huyo pia aliwahimiza wazazi kushirikiana na Idara za usalama kwa kuwaripoti wahalifu.