Kamati ya usalama kaunti ndogo ya Malindi imetoa tahadhari ya usalama kufuatia tishio la shambulizi la kigaidi mjini Malindi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo, Gideon Ombongi, kundi la kigaidi la Jaysh Ayman chini ya kiongozi wake Abdifatah Abubakar maarufu Musa Muhajir linapanga kutekeleza shambulizi ambalo limeorodheshwa kuwa shambulizi kubwa zaidi kufanyika humu nchini. 

Ni kufuatia tahadhari hiyo, Ombongi amewataka wananchi kuepuka sehemu zenye msongamano wa watu, sawia na kuwatahadharisha wamiliki wa nyumba za kupangisha kuwafahamu wapangaji wao, na kuwataka kutoa habari za watu wanaowashuku mienendo yao. 

Ripoti za ujasusi zinaonyesha kwamba Ayman tayari ametumwa mjini Malindi kutekeleza shambulizi hilo kwa ushirikiano na kundi la vijana, huku ripoti hizo za ujasusi zikisema kundi hilo la kigaidi ni moja la kundi la kijeshi la Al Shabaab. 

Aidha, Ombongi ameongeza kwamba polisi tayari wanaendeela kuwahoji washukiwa watatu wa ugaidi.