Wakimbizi 272 wa ndani kwa ndani waliobaki katika kambi ya Mumui mjini Subukia, Jumanne walikesha kwenye baridi ya mvua iliyonyesha Nakuru usiku kucha, wakihofia kufurushwa na utawala wa mkoa eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Taharuki ilianza kwenye kambi hiyo Jumanne jioni, baada ya ripoti za kukamatwa kwa mwenyekiti wao Samwel Chege Muchiri na maafisa wa CID mjini Subukia.

Akizungumza na mwandishi huyu kwa njia ya simu, Chege alisema “Nilikamatwa nikipeleka barua niliyotakiwa kuandika na Adan Wachu jijini, na nikazuiliwa katika ofisi za CID. Baadaye nilipelekwa katika ofisi za DO1 na DCIO wa Subukia, na nikaamrishwa kushirikiana na Chifu wa Mumui kuondoa IDPs wengine kambini”.

“Kila mtu amelala kwenye baridi kwa kuhofia kudhulumiwa na kufurushwa kwa nguvu,” Chege alisema.

Chifu wa kata hiyo Patrick Njung’e Jumatano alidhibitishia mwandishi huyu kwamba asubuhi alifika katika kambi hiyo, na kuwapa IDPs hao amri ya kuondoka kambini.

“Sijaruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari, japo mimi nafuata amri na nilikuwa kambini hapo saa moja asubuhi kuwapa ujumbe wa kuondoka kama nilivyotakiwa na wakubwa wangu. Naomba uzungumze nao” Njung’e alisema.

Muchiri amesema baada ya mkutano wa Afraha, serikali inafaa kuwatoa kambini humo wakimbizi wote pasi na kuwalazimisha.

"Tunaambiwa tuondoke, tutaenda wapi?" akahoji bwana Chege.

Hata hivyo DO1 wa Subukia Peter Yegon, alisema kwamba kulingana na stakabadhi za serikali na wizara ya mipango maalum, hakuna kambi ya wakimbizi iliyobaki nchini.

“Hakuna kambi ya IDPs hapa Subukia na taifa lote kwa jumla kulingana na stakabadhi za serikali. Mambo ya IDPs unaweza kupata ufafanuzi wake kutoka kwa Adan Wachu” akasema.

Hata hivyo alikataa kudhibitisha kama Chege alikamatwa Jumanne na maafisa wa CID.

“Mimi sijui kama alikamatwa au la. Kwani CID wakikamata mtu humleta kwa ofisi yangu? Kama alikamatwa, hayo sihusiki nayo”  Yegon alisema.