Hali ya taharuki imetanda kwa saa kadhaa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi mjini Mombasa Jumapili asubuhi baada ya ndege ya ufaransa kutua kwa ghafla kwa madai kuwa kuna bomu lililogunduliwa ndani yake.
Inasemekana kuwa abiria mmoja alielekea msalani na kisha akagundua kifaa alichoshuku kuwa bomu na baada ya rubani kupata taarifa hiyo alilazimika kutua kwa ghafla katika uwanja wa Moi.
Abiria wote waliokuwemo ndani walikaguliwa na kisha maafisa wa upelelezi pamoja na jeshi la wanamaji la Kenya kuikagua ndege hiyo kabla kuchukua kifaa hicho kwa uchunguzi zaidi.
Ulinzi mkali uliwekwa katika uwanja huo ambao hupokea ndege kutoka mataifa mbalimbali duniani huku abiria 2 waliohusishwa na kifaa hicho wakikamatwa na maafisa wa usalama ili kuhojiwa zaidi.
Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaiseri aliwasili saa kadhaa baadaye akiandamana na katibu katika wizara hiyo Monica Juma ambao walihutubia wanahabari na kusema kuwa serikali inaendeleza uchunguzi.
“Tumepokea hii habari na ndio maana tumefika hapa, tunawasihi watu kuwa watulivu idara ya usalama inafanya uchunguzi na tutatoa taarifa baadaye,” alisema Nkaiseri.
Hata hivyo abiria waliokuwa ndani walidinda kutumia ndege hiyo kuendelea na safari na kudai kuletewa ndege nyingine, hatua iliyofanya kupelekwa katika hoteli kadhaa za Mombasa wakingojea hatua zaidi kuchukuliwa.
Ndege hiyo aina ya Boeng 777 ilikuwa imetoka nchini Mauritius ikielekea mjini Paris Ufaransa na ilikuwa imebeba abiria 459 pamoja na wafanyikazi 14.