Gavana wa Mombasa Granto Samboja. [Picha: nation.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Granton Samboja anatarajiwa kuteua tena watu watatu ili kukamilisha baraza lake la mawaziri.

 Hii ni baada ya bunge la kaunti hiyo kukataa kuidhinisha majina ya watu wawili kati ya majina tisa ambayo yaliwasilishwa kupigwa msasa.

Wawili hao ni Everlyn Shighi Mngoda ambaye alipendekezwa kuongoza wizara ya huduma za umma na usimamizi na mhandisi Jefferson Mwakidisa aliyepaswa kuchukua kuongoza idara ya nyumba, miundo msingi na ujenzi.

Kulingana na kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti hiyo Jason Tuja, mhandisi Mwakidisa alichujwa kutokana na umri wake huku wengi wa wajumbe wa bunge hilo wakipendekeza gavana kuteua kijana badala ya mzee.

Shighi angali anafanya kazi katika kitengo cha kaunti cha huduma kwa umma. Hata hivyo hapakuwa na sababu kamili ya jina lake kutoidhinishwa.

Mmoja kati ya wale gavana Samboja alikuwa amependekeza kuchukua nafasi za uwaziri alijiondoa akisema ana majukumu mengi ambayo yatamzuia kuhudumu katika afisi hiyo.

Walioidhinishwa ni Claris Mnyambo wa ardhi na mazingira, Bigvai Mwailemi ambaye atasimamia idara ya vijana, michezo na masuala ya kijamii, Getrude Nawoti atakaye ongoza wizara ya biashara na utalii  na Davis Mwangoma wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Wengine ni daktari Frank Mwangemi ambaye sasa ndiye atakayeongoza sekta ya afya katika kaunti ya Taita Taveta, Daniel Makoko Mwakisha ambaye atasimamia sekta ya elimu na daktari Vincent Masawi ambaye atasimamia sekta ya fedha na mipango.

Masawi alihudumu katika serikali iliyotangulia chini ya gavana John Mruttu na atasimamia wizara hiyo kwa awamu ya pili.