Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara wameipongeza serikali ya kaunti ya Nyamira kwa juhudi zake za kulisafisha soko la Keroka.

Hii ni baada ya wafanyibiashara wa soko hilo kuandamana siku ya jumatatu wiki jana wakilalamikia ukosefu wa huduma ya kutoa taka, kutokarabatiwa kwa soko hilo pamoja na barabara mbovu.

Sasa magari ya kaunti yameanza kuzoa taka hizo ambazo zilikuwa zimetapakaa kila pahali, jambo ambalo limepelekea serikali ya kaunti hiyo kupongezwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya jumapili,wafanyibiashara hao wakiongozwa na Gladys Bosibori, waliipongeza serikali ya kaunti kwa kuitikia wito wao na kuanza kuondoa uchafu huo.

“Tunaona uchafu uliokuwa unatusumbua hapa Keroka asa umeanza kutolewa na tunaishukuru sana serikali ya kaunti. Kile tunachohitaji ni wahudumu wa kuzoa taka wawekwe katika soko hili ili wawe wanatoa uchafu huo mara kwa mara ili tusiwe tunalalamika tena,” alisema Bosibori.

Aidha, wafanyibiashara hao wameapa kutotozwa ushuru hadi wajengewe vyoo vipya ili kuimarisha mazingira katika soko hilo.

“Hakuna siku tutaruhusu watoza ushuru kuja hapa Keroka kututoza ushuru hadi tujengewe vyoo vipya na tukarabatiwe soko kisawasawa. Baada ya hapo, tutaweza kufikiria mambo ya ushuru,” aliongezea Brighton Omariba.