Tamaduni za kale miongoni mwa jamii ya Pwani sawa na ukosefu wa elimu ni sababu msingi zinazopelekea ndoa za mapema miongoni mwa wasichana wadogo katika ukanda huu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mkurugenzi wa shirika linalowasaidia wanawake wanaoteseka kisaikolojia la ‘Solidarity with Women in Distress’ yaani Solwodi Ruth Lewa alisema kwamba swala hilo limekithiri mno katika sehemu za mashambani, huku wazazi wengi wakishikilia mila za kuwaoza mabinti zao mapema huku wakiwasomesha watoto wao wakiume pekee.

Akizungumza katika afisi za shirika hilo mjini Mombasa na mwanahabari huyu, afisa huyo wa maswala ya kijinsia na haki za wanawake na watoto nchini alisema kuwa hali hiyo imesababisha pengo kubwa katika jamii, huku watoto wa kike wakikosa elimu na kulazimishwa kuanza familia mapema badala ya wazazi kujitahidi na kuwapatia elimu sambamba na wale wa kiume.

"Tumeona idadi kubwa ya watoto wakiolewa mapema kufuatia ukosefu wa msingi wa elimu katika jamii na hali hiyo lazima isitishwe ili kumlinda mtoto wa kike na tunapanga kufanya hamasa kwa jamii na mambo hayo yatasitishwa," alisema Ruth.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa hamasa mashinani na serikali za kaunti zote sita hapa Pwani kuchukua jukumu la kuihamasisha jamii kuhusiana na umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike na kumkinga mtoto huyo dhidi ya ndoa za mapema.