Kampuni ya maji ya Mombasa imesema kuwa imetatua tatizo la maji ambalo limekuwa likikumba maeneo ya Barsheba na Kisauni mapema wiki hii.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatano, afisa wa mawasiliano wa kampuni hiyo Sarah Langa’t, alisema tatizo hilo lilitokana na hitalifu za kimitambo zilizosababishwa na kupotea kwa nguvu za umeme katika eneo la Baricho, ambapo mitambo za kambuni hizo zinapatikana.

“Ni kweli kulikuwa na tatizo la maji kuanzia siku ya Jumatatu lakini hivi sasa shida hiyo imetatuliwa. Tumezungumza na kampuni ya Kenya Power na tayari wamerekebisha hitilafu iliyotokea,” alisema Lang’at.

Aidha, usimamizi wa bodi ya maji ukanda wa Pwani umesema ukarabati wa bomba la kusafirisha maji katika maeneo ya magharibi ya Pwani umekamilika na kuwa wakaazi watapata huduma za maji kama kawaida.

Haya yanajiri baada ya wakaazi wa eneo la Kisauni na Barsheba kulalama mapema wiki hii kufuatia ukosefu kwa maji, hali iliyowalazimu kutumia maji ya kisima.