Huenda uhaba wa maji katika Kaunti ya Mombasa ukapata suluhu la kudumu baada ya wakurugenzi wakuu wa kampuni ya usambazaji maji ya Mombasa kufanya kikao cha dhararu na serikali ya kaunti hiyo.
Mkurugenzi wa bodi ya kampuni hiyo Nick Munyi, amesema kuwa kikao hicho kimeafikiana vyema na shughuli ya usambazaji maji kwa wakaazi utarejea wakati wowote, baada ya mgogoro wa deni la shilingi milioni 600 kusuluhishwa.
Akiongea na wanahabari afisini mwake siku ya Jumatato, Munyi alisema kuwa deni hilo la shilingi milioni 600 ni kati ya malimbikizi ya madeni ambayo kampuni hiyo inadai serikali kuu na baadhi ya taasisi za serikali.
Alisema kuwa hali hiyo ilichangia kampuni hiyo kutofikia viwango vyake vya ukusanyaji ushuru.
Munyi amewataka wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kuwa na subra, na kuongeza kuwa mgogoro ambao ulisababisha uhaba wa maji kuingia wiki ya pili sasa unashughulikiwa, na wakazi watapata maji bila ya vizuizi vyovyote.
"Tunawahakikisha wakaazi wa Mombasa kuwa tatatizo la uhaba wa maji limesuluhishwa na maji safi yataanza kusambazwa katika maeneo ya makaazi wakati wowote kuanzia siku ya Jumatano wiki hii,” alisema Munyi.
Bodi ya huduma za usambazaji maji Pwani, 'Coast Water services Board' ilifunga mabomba yake ya usambazaji maji ya eneo la Baricho, Mzima, Tiwi na Marere, na Kaunti ya Mombasa, kufuatia malimbikizi ya madeni ambayo kampuni ya usambazaji maji Mombasa haikuwa imelipa.