Serikali ya kaunti ya Nakuru imeanzisha mradi unaonuia kuwaimarisha vijana kiuchumi, kwa ushirikiano na kampuni moja ya Japan.
Ushirikiano huu utawapa vijana hawa mafunzo ya mbinu mpya ya kukarabati barabara za mashinani, maarufu kama Do-nou Technology.
Mradi huo umeanzishwa katika wadi ya Bahati na vijana wanafunzwa jinsi ya kutengeneza barabara kwa kutandika magunia yenye mchanga chini kwanza, kisha wanamwaga changarawe juu ya magunia hayo na hatimaye kusindilia.
Kulingana na mwakilishi wa wadi ya Bahati Peter Nderitu, vijana hao waliochaguliwa kutoka lokesheni zote za wadi hiyo, hatimaye watajiunga katika kikundi kimoja na kusaidiwa na serikali ya kaunti kusajili kampuni yao ya ukarabati wa barabara.
“Watakuwa katika nafasi ya kwanza kufaidika na kandarasi ambazo zinatolewa na serikali ya kaunti, wakisajili kampuni, na tayari wameanza kupata mafunzo manake barabara moja katika wadi yangu imetengenezwa kwa teknolojia hiyo,” alisema Nderitu.
Kando na kuwapa ajira vijana hao, serikali ya kaunti itapunguza gharama ya kukarabati barabara hizo kila mwaka ama baada ya msimu wa mvua. Kulingana na Nderitu, barabara iliyoudwa kwa teknolojia ya Do-nou hukaa zaidi ya miaka mitatu bila ya kukarabatiwa upya.
“Kama kaunti ambapo ukulima unatiliwa mkazo, ni lazima tuwe na namna ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika kila wakati. Iwe jua iwe mvua,” alisema Nderitu ofisini mwake.