Kuna uwezekano kuwa vijana wa kurandaranda mjini Eldoret wanasajiliwa katika kundi la kigaidi la al-Shabaab, spika wa bunge la kaunti ya Uasin Gishu Isaac Terer Ijumaa amesema.
Terer ameitaka idara ya usalama mjini Eldoret kuchunguza fununu hizo huku akionya kwamba iwapo uvumi huo utapuuzwa kuna hatari ya kundi hilo kuanza kutekeleza uhalifu mjini Eldoret.
“Ninaomba idara ya usalama kuziba mianya yoyote inayoweza kufanya vijana kusajiliwa katika kundi la kigaidi la al-Shabaab,” alisema.
Terer alisema hayo katika bunge la kaunti ya Uasin Gishu ambapo aliwaomba vijana wawe wazalendo.
Aliwaomba wakazi kuwa waangalifu zaidi na kuripoti mtu yeyote ambaye wanashuku kwa maafisa wa usalama.
“Ni bayana kuwa yeyote ambaye amesajiliwa kuingia kwenye kundi la al-Shabaab ni tishio kubwa kwa wananchi kwa hivyo ni jukumu la wananchi kuripoti watu hao kwa maafisa wa polisi,” aliongeza.
Madai ya Terer yamewadia siku chache baada ya hofu kutanda katika chuo kikuu cha Moi kuhusiana na madai kuwa kundi la al-Shabaab linatishia kuvamia chuo hicho.