Siku chache baada ya tahadhari kutolewa kuhusiana na kuchipuka kwa maradhi ya homanyongo katika baadhi ya mitaa katika Kaunti ya Mombasa, idara ya maji kwenye Kaunti hiyo imetangaza rasmi kuanza kuwachunguza wamiliki wa hoteli, wachuuzi wa chakula, pamoja na kampuni za kupakia maji ya chupa, ili kuepusha wenyeji na maradhi hayo.
Kwenye mahojiano na waandishi wa habari siku ya Jumanne jijini Mombasa, mkuu wa idara ya maji katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya alitoa onyo kwa wenye kampuni za maji ya chupa kuwa serikali ya Kaunti itaanza kuchunguza biashara hiyo ambayo kwa sasa imekita kwenye kila mitaa jijini Mombasa.
Thoya alisema kuwa washikadau kwenye biashara hizo wamechukua nafasi hiyo kujifaidi na wengine hata huenda wanapakia maji hayo kwenye chupa bila kuzingatia usafi na afya za wateja na watumiaji wa bidhaa zao.
Mkuu huyo wa idara aidha alisema kuwa kuna uwezekano kuwa watu wengine wanatumia maji ya visima na mbinu zisizo na utalaam wa kufikia viwango hitajika vya kupakia bidhaa za maji.
Alitoa wito kwa wakaazi kwa jumla kuzingatia usafi na pia kuhakikisha kuwa maji pamoja na vyakula wanavyokula ni safi, ili kujiepusha na maradhi hayo.