Serikali ya kaunti ya Lamu imeahidi kuajiri maaskari 20 wa kaunti hiyo kufikia mwezi ujao ili kukabiliana kikamilifu na walanguzi na watumizi wa mihadarati katika kaunti hiyo.
Kulingana na gavana wa kaunti ya Lamu Issah Timamy, vitengo vya usalama vilivyotumwa na serikali kuu kushika doria katika kaunti hiyo kamwe hawajatekeleza jukumu lao vyema hasa katika kuwakabili walanguzi wakuu wa mihadarati.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, Gavana Timamy amesema kuwa maaskari yao watazuru nyumba hadi nyumba katika juhudi za kukabiliana na biashara hiyo haramu ili kuona kuwa kaunti hiyo inawanasua vijana waliadhirika.
Timamy amelaumu vitengo vya usalama vilivyokita kambi katika kaunti hiyo kwa kukosa kuwajibika katika utendaji kazi na akasema kuwa iwapo swala hilo katika kisiwa cha Lamu na kaunti nzima kwa jumla halitakabiliwa basi vijana wengi wataangamia.
"Vitengo vya usalama vilivyotumwa Lamu hakuna hata mlanguzi mmoja tumeona akitiwa mbaroni na kwa sababu hiyo wameonyesha wazi wameshindwa kuzuia mihadarati ndio sisi kama kaunti ya Lamu tumeamua kuajiri maafisa wetu kukabiliana na hali hiyo," alisema Timamy.
Kiongozi huyo ametoa wito kwa wakaazi kushirikiana ili kwa pamoja kukomesha tatizo hilo ambalo limeathiri vijana wengi na kurudisha nyuma maswala ya kimaendeleo katika kaunti hiyo.