Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko anapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kuachiliwa huru kwa washukiwa wawili waliokuwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya watu 60 katika eneo la Mpeketoni, Kaunti ya Lamu.
Katika taarifa aliyoitoa, Tobiko alisema kuwa atakata rufaa ndani ya kipindi cha siku 14 ili kupinga uamuzi huo uliotolewa siku ya Jumatano.
Alisema kuwa hajaridhishwa na uamuzi huo uliotolewa na jaji Martin Muya wa mahakama ya Mombasa.
Aidha, aliongeza kuwa anataka wawili hao kuhukumiwa kifo kwa mujibu wa sheria.
Siku ya Jumatano, mahakama kuu ya Mombasa iliwaachilia huru Diana Salim na Mahadi Swaleh baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.
Wawili hao wanadaiwa kuhusika katika mauaji hayo yaliyozua hali ya taharuki katika Kaunti ya Lamu kati ya tarehe Juni 15 na 17 mwaka 2014.
Jaji Martin Muya alisema ushahidi wa mashahidi 32 wa kesi hiyo hauambatani hivyo basi ni vigumu kuwahusisha wawili hao na mauaji ya Mpeketoni na Kaisari.
Aidha, aliongeza kuwa maafisa wa upelelezi walishindwa kufanya uchunguzi wa kutosha.