Muungano wa kutetea waalimu wa shule za upili na vyuo vya kadiri (KUPPET) umesema kuwa tume ya kuwaajiri walimu (TSC) inawasukuma walimu kufanya mgomo mwaka ujao kwa kuwalazimu kutia sahihi kandarasi za utendaji kazi.
Mwenyekiti wa KUPPET tawi la Nakuru Njau Kuria amesema kuwa TSC imezidi na inapaswa kunyamazishwa.
Akiongea Jumatatu mjini Nakuru, Kuria alisema kuwa walimu kamwe hawatatia sahihi kandarasi za utenda kazi na wataitisha mgomo iwapo TSC itasisitiza jambo hilo.
"Hii TSC imeshindwa na kazi na wanachofanya ni kuwachokoza walimu na kuwalazimu kuitisha mgomo na sisi tuko tayari kwa hilo," alisema Kuria.
Aidha, Kuria aliwaonywa walimu wakuu wa shule dhidi ya kuwalazimu walimu walio chini yao kutia sahihi kandarasi hizo kutoka TSC.
"Walimu wakuu wasikubali kutumiwa na TSC kuwadhulumu walimu na kandarasi kwa kuwa hili halitakubalika na walimu wakuu wafahamu hivyo," aliongeza Kuria.