Tume ya kuajiri walimu nchini TSC imezindua rasmi sheria zitakazothibiti utendakazi wa walimu, mwongozo wa maadili pamoja na mikakati yake ya mpangilio wa miaka mitano kutoka mwaka 2015-2019.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa tume hiyo Lydia Nzomo amesema sheria hizo zitasaidia pakubwa kuboresha utendakazi wa walimu nchini na kuifanya taaluma hiyo kuwa na hadhi, baada ya kile alichokitaja kama taaluma hiyo kudharauliwa kwa muda mrefu.

Akizundua rasmi mwongozo huo siku ya Jumatatu katika hoteli moja jijini Mombasa kwenye hafla iliyohudhuriwa na washikadau wa elimu, Nzomo alisema kuwa sheria hizo zitawezesha walimu wote katika shule za umma na za kibinafsi kusajiliwa na tume hiyo ambapo orodha ya kila mwaka ya walimu waliosajiliwa itakuwa ikichapishwa.

Vile vile, sheria hizo zinaeleza kukabiliana na unyanyasaji wa kimapenzi wa walimu dhidi ya wanafunzi, hatua za kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya shuleni pamoja mwongozo kuhusu masomo ya likizo.

Hata hivyo, walimu waliokuwa wamehudhuria kongamano la 41 la walimu wakuu wa shule za upili nchini linaloendelea mjini Mombasa, wakiongozwa na Katibu wa chama cha walimu nchini Knut tawi la Kilindini Dan Aloo, walikosoa sheria hizo mpya.