Mavazi ni njia mojawapo tunayostahili kutumia kutunza utamaduni wetu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Jamii ya Mijikenda ina mavazi ambayo yanahifadhi mila na desturi ya Pwani.

Hando ni vazi la kitamaduni la wanawake wa Kimijikenda, ambalo lazima lilindwe kwa minajili ya vizazi vijavyo.

Hili vazi linastahili kuwa refu hadi magotini ili kusitiri sehemu za siri kama njia ya kuonyesha heshima.

Vazi hili linatengenezwa na pamba na ni muhimu sana kwa jamii hii na huvaliwa kila mahali.

Wakati mwingine, hando huvaliwa wakati wa sherehe maalum.

Kuna aina ya hando iitwayo bandika, ambayo huwa fupi kuliko honda ya kawaida na huwa na rangi nyingi. Bandika huvaliwa nyumbani na katika densi.

Vazi hili husaidia mabinti kunengua viungo na kuonyesha sehemu za mwili kama vile paja.

Hata hivyo, mwanamke anapoenda pahala panapohitaji heshima, anastahili kuvaa leso juu ya bandika.

Kila rika la wanawake laweza vaa hando lakini kuna masharti kulingana na aina ya rangi.

Tune ni hando nyekundu. Hili ni vazi la wanawake walio na roho fulani. Rangi za samawati na nyeupe zinaweza kuongezwa na pia hirizi kuvaliwa.

Hando nyeupe linaitwa bafuta na linatumika harusini bila masharti ya rika.

Vile vile, hando ramsimbiji ni honda la samawati na huvaliwa na watu wenye uwezo wa kuponya kitamaduni.

Hando rakaputula ni aina nyingine ambayo ni fupi na huwa na rangi tofauti tofauti.

Hando huvaliwa na mapambo mengine. Waeza ongeza tunda, vivorodete, mkufu, tsango, vidanga na vifufu.