Gavana wa Jimbo Nakuru Kinuthia Mbugua amewataka wanasiasa katika jimbo la Nakuru kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha maendeleo.
Akizungumza katika shule ya upili ya Akusi katika eneo bunge la Solai siku ya Jumamosi, Mbugua alisisitiza umuhimu wa umoja baina ya wanasiasa.
Mbugua alisema kwamba maendeleo ni jukumu la kila mwanasiasa aliyechaguliwa na wananchi wa Nakuru.
“Wanasiasa katika jimbo hili hawana budi ila kufanya kazi kwa pamoja ili tuimarishe utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi,” alisema Mbugua.
Kiongozi wa Jimbo pia aliwaomba wanasiasa kukoma kutumia maneno ambayo yatazua uhasama baina ya raia, akiongezea kwamba wakati umefika wa wanasiasa wachochezi kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mbugua alisema kwamba jimbo lake halitawakaribisha wanasiasa ambao wanaendeleza uchochezi wa kiukabila.
Gavana Mbugua, ambaye alikua akiongoza harambee kwa minaajili ya ujenzi wa kanisa la Kikorino katika eneo la Solai alisema kwamba wakati umefika wa wanasisasa kuhudumia wakenya.
Wakati huo huo, Mbugua alisisitiza kwamba serikali yake imeweka mikakati mwafaka kuhakikisha wananchi wanapata huduma. Aliongeza kwamba miradi mbali mbali imeanzishwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Kuhusiana na swala la usalama wa kitaifa, Mbugua aliiomba serikali kuu keweka mikakati muhimu ambayo itahakikisha usalama wa wananchi.
Mbugua aliwasuta viongozi ambao wanamkashifu raisi Uhuru Kenyatta kuhusiana na usalama, akisema ni jukumu la kila mwananchi kuchangia kewepo kwa usalama.
Hata hivyo, Mbugua aliziomba idara kuu za usalama nchini kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kusitisha visa vya uhalifu na ugaidi ambavyo vinazidi kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini.
“Ombi langu ni kwa idara za ujasusi kufanya kazi kwa pamoja ili kukabiliana na uhalifu,” alisisitiza Mbugua.