Sekta ya utalii mjini Mombasa imeelezea kero yake dhidi ya ongezeko la tuktuk mjini humo ikidai kwamba zinaathiri ukuaji wa sekta hiyo.
Inadaiwa kuwa tuktuk hizo ambazo zinaongezeka kila siku zinasababisha msongamano mkubwa mjini na kuharibu taswira ya mji huo wa kitalii.
Akizungumza kwenye mkutano na washikadau wa utalii eneo hilo, mwenyekiti wa muungano wa maslahi ya watalii Pwani Mohamed Hersi, alisema tuktuk ni kero kubwa tofauti na vile watu wanavyoamini kwamba zinakuza uchumi.
“Kuna imani kwamba kadri tunavyoziongeza tuktuk ndivyo tunavyotoa fursa za kazi. Kile tunakosa kutambua ni kwamba tunafukuza kabisa watalii kutoka eneo hili,” alisema Hersi.
Hersi alichukua nafasi hiyo kutoa wito kwa idara ya uchukuzi katika Kaunti ya Mombasa kuweka mikakati ya kupunguza tuktuk hizo.
Pia aliitaka wizara hiyo kusitisha zoezi la kusajili tuktuk zaidi kama njia moja ya kutatua tatizo hilo.
“Tunahitaji tuktuk lakini hatuwezi kusajili zaidi. Huu ni mji wa kitalii na tunataka kuona wawekezaji wakikuja kwa wingi,” alisema Hersi.
Kulingana na mwenyekiti huyo ni kwamba hapo awali mji huo ulikuwa na jumla ya tuktuk elfu tatu kisha zikaongezeka hadi elfu saba, na sasa zimefika elfu 11.
Iwapo pendekezo hilo litatekelzwa, huenda likaathiri pakubwa sekta ya uchukuzi mjini Mombasa kwani usafiri wa tuktuk unategemewa na watu wengi zaidi.