Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar ameshikilia msimamo wake kuwa atawania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 licha ya kupata shinikizo ya kujiondoa katika kinyang'anyiro cha ugavana.
Akihutubia kongamano la viongozi wa vijana katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumanne, Hassan aliwashauri vijana kujitokeza ili kuwania nyadhfa za uongozi bila ya kuogopa mtu yeyote.
“Kuna watu wengi wametumwa kwangu wengine hata na pesa ili waniambie nijitoe katika kuwania ugavana lakini mimi nawambia kila mara tukutane 2017 kwa debe,” alisema Omar.
Seneta huyo ameonekana siku za hivi majuzi akikashifu serikali ya kaunti ya Mombasa inayoongozwa na gavana Joho akisema kuwa haina miradi yoyote ya Maendeleo.