Kiongozi wa muungano wa Cord Raila Odinga amedai kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imetia sahihi ya maelewano na serikali ya Jubilee kuhakikisha serikali hiyo imerudi mamlakani katika uchaguzi ujao wa mwaka 2017.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumapili usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, Odinga alisema yeye amefanya uchunguzi na kubaini njama inayoendelea kati ya serikali iliyoko mamlakani na tume ya IEBC.

“kufikia sasa najua yale yanaendelea serikalini na tume ya IEBC wanataka kuhakikisha Jubilee imerudi mamlakani katika uchaguzi ujao,” alisema Odinga.

“Serikali wameelewana na makamishina wa tume hiyo kwamba wakichukua uongozi tena na makamishina hao watastaafu kisha kuchaguliwa na serikali hiyo katika nyadhifa mbalimbali ili kuhakikisha lengo na ndoto zao zimetimizika,” aliongeza Odinga.

Aidha, Odinga alisema liwe liwalo Cord hawatashiriki katika uchaguzi ujao ikiwa makamishina hao hawataondoka kwani hawana imani nao.

“Sisi WanaCord tutaendelea na maandamano kuhakikisha makamishina hao wamejiondoa au kuondolewa,” alisisitiza Odinga.