Wakaazi wa Koru kwenye Kaunti Ndogo ya Muhoroni wameiomba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusambaza huduma za zoezi la usajili wa wapiga kura hadi kwenye maeneo ya mashambani ili kuwafikia wakenya wote.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi hao walihoji kuwa zoezi hilo ambalo linaendelea katika Kaunti ya Kisumu linakaribia kumalizika huku wakenya wengi katika Kaunti hiyo wakiwa hawajajisajili kama wapiga kura.

Anjelina Akumu ambaye ni mfanyibiashara katika soko la Koru aliomba tume hiyo kusambaza vituo kadhaa kwenye maeneo ya shule na soko ili kuweza kuwafikia wakaazi ambao ni wakongwe na walemavu.

“Tunao walemavu wengi sana ambao hawajapata kupiga kura kwa miaka mingi kwa sababu za kukosa kujiandikisha kama wapiga kura, huku wazee wakongwe nao wakishindwa pia vile vile kufikia maeneo ya usajili,” alisema Akumu.

Aidha, wakaazi hao walitaka muda uliowekwa kwenye awamu inayoendelea kwa sasa kuongezwa ili kuwepo na usawa kwenye zoezi hilo kwa kumfikia kila mwananchi.

Wakiongea kwenye kikao cha mafunzo ya uma yaliyoandaliwa na Shirika la Ecumenical Centre for Justice and Peace Tawi la Kisumu yaliyoongozwa na Mkurugenzi wake Elias Komenya, wakaazi hao waliitaka tume hiyo pia kuhamazisha wananchi kupitia vyombo vya habari na mashirika yanayotoa elimu ya uma nchini kabla ya kuanzisha shuhguli kama hiyo.

Uandikishaji wa wapiga kura unaendelea katika Kaunti ya Kisumu lakini kwa sasa unafanyika kwenye afisi za IEBC pekee ambapo wachache tu ndio wanaoendelea kujitokeza kusajiliwa.

Mkurugenzi Komenya alisema kuwa atafikisha maombi yao kwa tume hiyo ili kusambazwa zoezi hilo kwenye shule na soko zilizo karibu na watu wengi.