Tume ya kitaifa ya usawa wa jinsia imesema kwamba itaangazia njia mpya za kupigania swala la uwakilishi sawa wa kijinsia katika uongozi nchini ili kuhakikisha kwamba katiba inazingatiwa kikamilifu.
Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Winfred Lichuma, kuangushwa kwa mswada huo bungeni siku ya Alhamisi ni pigo kubwa sio tu kwa wanawake humu chini bali pia jamii hasa ikizingatiwa kwamba wanawake, vijana na jamii ya walemavu wamekosa uwakilishi katika nafasi mbalimbali serikalini.
Kwenye taarifa yake aliyotumwa kwa wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Lichuma amesema kwamba uzembe huo wa bunge la Kitaifa unalirudisha nyuma taifa hili na huenda Kenya ikakumbwa na msukosuko wa kikatiba iwapo uchaguzi mkuu ujao utawapeleka wanaume wengi katika mabunge yote mawili ya Seneti na lile la Kitaifa huku wanawake wakizidi kuwachwa nyuma katika maswala ya kiuongozi.
Mwenyekiti huyo wa tume ya usawa wa kijinsia nchini amewataka wadau wote kuungana na kujadili jinsi mswada huo utakavyopenya na kupitishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba katiba inazingatiwa kikamilifu huku akihoji kwamba wanawake humu nchini hawapaswi kukata tamaa kutokana na matokeo ya hapo jana bungeni.
"Tunawaka wadau wote wakupigania usawa wa jinsi nchini kuhakikisha kuwa wanaungana na kujadili jinsi mswada huu utakavyowasilishwa tena mbungeni na kupitishwa ili wanawake wawezekuwakilishwa vyema bungeni na katika idara mbalimbali nchini," alisema Lichuma.
Siku ya Alhamis kwa mara ya pili tena bunge la kitaifa lilishindwa kupitishwa mswada wa kuongeza idadi ya wanawake katika uwakilishi bungeni baadhi yao wakidai kwamba mswada huo utamuongezea mzigo wa ushuru Mkenya mashinani.