Walimu kutoka eneo la Masaba Kaskazni wameiomba tume ya kuwaajiri walimu (TSC) kuwajali wakati wa kuwahamisha hadi shule zingine.
Akiongea siku ya Jumatano akiwa eneo la Masaba Kaskazini katika Kaunti ya Nyamira, mwenyekiti wa walimu kutoka Masaba Meshack Obonyo ameiomba TSC kuzingatia afya na masuala mengine ya walimu kabla ya kuwahamisha kuenda katika shule zingine.
Kwa mujibu wa Meshack, walimu uhamishwa kuenda katika shule zingine ambazo ni mbali kutoka sehemu wanakoishi, jambo ambalo amesema huwa ngumu kwa walimu hao kwani kiwango cha pesa wananachokabidhiwa cha marupurupu ni kidogo mno ambacho hakiwatoshi katika shughuli zao za kila siku.
“Walimu hupata mshahara ambao ni wa kiwango cha chini na wakati wanahamishwa kwenda katika shule za mbali huwa wanapitia shida kubwa kwa kuwa hawana pesa za kutosha ambazo wanazitumia kama nauli ya kusafirisha bidhaa zao zote,” alihoji Meshack.
Aidha, ameiomba tume hiyo kuzingatia masuala ya walimu kwa kina ili kuwasaidia na kuwapokeza pesa watakazozitumia kujiendeleza kimaisha.
Alisema kuhamishwa kwa baadhi ya walimu kutoka Keroka kuenda Risa, Riamoni na Gesima ambazo ziko mbali kutoka Keroka mahali walikuwa wakifundisha ni kuwatesa walimu hao.
Kwingineko, mwekahazina Evans Karuru ameiomba tume hiyo kuzingatia afya ya walimu pia kabla ya kuwahamisha hadi shule zingine za maeneo mbali.