Tume ya uiano na utangamano nchini imehimizwa kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wanaokiuka sheria na kueneza matamshi ya chuki na uchochezi miongoni mwa jamii.
Akiongea na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Jumanne, katibu mtendaji wa baraza la maimamu na wahubiri wa humu nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa amesema kuwa hali hiyo isipothibitiwa, basi huenda kura za uchuguzi mkuu wa mwaka ujao zikavurugika.
Sheikh Khalifa anapendekeza tume ya NCIC kuwajibikia majukumu yake jinsi ipaswavyo na kudhibiti hali hiyo kwani viongozi wa kisiasa sasa wamebadilika na hata kupigana hadharani kutokana na kukosa nidhamu.
“Tunawaambia makamishna wa tume ya NCIC kuwajibikia majukumu yao na kuwachukilia hatua viongozi wachcohezi kwani imekuwa tabia hawaogopi tena na kutukanana hata kupigana hadharani, hiyo sisi hatutakubali, lazima NCIC ichukue hatua,” alisema Sheikh Khalifa.
Kiongozi huyo wa kidini sasa anawashinikiza wakazi kujitenga na viongozi kama hao kwani hawatawaleta mabadiliko yoyote ya kimaendeleo na demokrasia bali kuvuruga amani ya taifa hili.
Picha: Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa humu nchini CIPK Sheikh Mohammed Khalifa. Anapendekeza viongozi wachochezi kuadhibiwa.