Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hatua ya kutengewa kiwango kidogo cha fedha kwa tume ya kitaifa wa ardhi, NLC, imetatiza utoaji wa huduma mwafaka.

Huo ni usemi wa mwenyekiti wa tume hiyo Muhammud Swazuri aliyekuwa akizungumza mjini Nakuru jumanne wakati wa mkutano wa majadiliano na maafisa wa ardhi kutoka kwa kaunti mbalimbali.

Kwa mujibu wa Swazuri, katika mwaka wa kifedha wa 2014-15, tume hiyo iliomba itengewe shilingi bilioni nane lakini ilipata shilingi bilioni mbili pekee.

Aliongeza kwamba katika mwaka wa kifedha wa 2015-16, tume hiyo iliomba itengewe shilingi bilioni saba nukta mbili lakini ilipata shilingi bilioni moja nukta nane pekee.

"Tulitengewa fedha chache mno katika miaka hiyo miwili ya kifedha. Milioni nne katika miaka hiyo miwili ya kifedha ilikuwa itumike kwa makaazi. Katika kaunti ya Nakuru, tuna maelfu ya watu ambao tunahitaji kuwapa makaazi,’ alisema Swazuri.

Mwenyekiti huyo aliashiria kuwa tume hiyo inahitaji kuwapa watu makaazi katika kaunti mbalimbali kama vile Kajiado, Nakuru na Narok kupitia kwa makaazi hayo.

Hata hivyo, alieelezea imani yake kwamba kupitia kwa ushirikiano mpya kati ya wizara ya ardhi na tume yake, huenda wakapata fedha wanazohitaji.

Wakati huo huo, aliangazia swala la fedha kutoka kwa wadau wengine akisema washirika hao kwa wakati mwingine hukosa kutoa fedha kutokana na mizozo ya ndani kwenye wizara ya ardhi. 

Licha ya hayo, alisema kwa ushirikiano na wizara ya ardhi, wataweza kuhakikisha huduma zao zote zinapatikana kupitia kwa njia ya mtandao, hatua ambayo itahakikisha kuna ubora katika utoaji wa huduma zao.

"Tunaangazia pia umuhimu wa uwekaji kwenye tarakilishi rekodi zetu, hatua ambayo ni miogoni mwa majukumu ya tume ya ardhi. Kabla ya baraza la mawaziri kugeuzwa, tulikuwa tumekubaliwana na aliyekuwa waziri wa ardhi kuweka rekodi hizo kwenye tarakilishi ili tuweze kubaini wamiliki wa mashamba," aliongeza Swazuri. 

Kwa upande mwingine, amekariri kwamba tume hiyo ya ardhi imepasta mashini zenye thamani ya shilingi milioni 50 akiongeza kwamba mashini zingine zitanunuliwa ili kuweza kukamilisha hatua ya kuweka huduma zao kwa njia ya kisasa ya kidijitali kama vile ada zinzotozwa kwenye vipande vya ardhi na ada zinaoztozwa endapo mtu anataka kukodi kipande cha ardhi.