Baadhi ya wakazi wa mji wa Kisii wameiomba kampuni ya kutoa huduma ya umeme (Kenya Power) kushughulikia tatizo la umeme kukatika katika mji huo kila mara.
Wakiongea siku ya Ijumaa na Mwaandishi huyu katika mji wa Kisii, wafanyibiashara katika mji huo walisema wanakadiria hasara haswa kwa biashara zinazotumia umeme kutokana na kukatika kwa umeme kila mara.
Walisema kuwa wiki uliopita walikadiria hasara kubwa kutokana na ukosefu wa umeme katika maeneo yao ya biashara licha ya kulipia huduma hiyo.
Kwa sasa wameiomba kampuni ya nguvu za umeme katika mji wa Kisii kushughulikia na kutatua shida hiyo haraka iwezekanavyo ili kuzuia hasara zaidi na pia kama njia moja ya kuinua viwango vya uchumi katika kaunti ya Kisii.
Mfanyibiashara mmoja wa kuchapisha katika mji huo Viviana Moraa, alisema yeye hukosa wateja wengi sana haswa kutokana na hali hiyo, inayomlazimisha kutumia gharama zaidi ya kutafuta nguvu mbadala, hali ambayo alisema imempeleka hasara kubwa.
Kampuni zingine zinazotengeneza bidhaa katika mji wa Kisii pia ziliunga mkono wakazi hao nakusema kuwa wakati umeme haupo watu ukosa kazi katika kampuni hizo kando na kupata hasara.
“Wakati umeme haupo katika mji wetu wa Kisii kama leo hii, tunakadiria hasara kubwa na tunaomba kampuni ya kusambaza umeme kutatua shida hili ili tuweze kuendelea na biashara yetu," alihoji Nelson Nyaata, mfanyibiashara wa kuuza Soda katika mji wa Kisii.