Viongozi wa kisiasa kutoka kaunti ya Kisii wameitaka serikali ya Jubilee kutumia hela zinazotumika katika idara ya huduma kwa nchi kulipa walimu ambao wamegoma badala ya serikali kudai kuwa hawana hela.
Viongozi hao zaidi ya kumi walishangaa ni kwa nini walimu wanaendelea kudhulumiwa hata baada ya mahakama kuu kutoa uamuzi kuwa wapatiwe nyongeza ya kati ya asilia mia 50 na 60, huku wanafunzi wakiendelea kupoteza mda mwingi ikizingatiwa kuwa baadhi yao wanaenda kufanya mitihani ya kitaifa.
Wakiongozwa na mbunge wa Borabu Ben Momanyi katika hafla moja ya iliyofanyika katika uga wa michezo wa Gusii siku ya Jumamosi, viongozi hao walidai kuwa serikali ina hela ya kutosha ya kulipa walimu, ikizingatiwa kuwa serikali inapata ushuru kutoka kwa kila mkenya, walimu wakiwa ni miongoni mwao, na ni haki yao kupata nyongeza hiyo.
Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong’i, ambaye alisema hela ambazo zinaendelea kutumiwa vibaya na baadhi ya wizara na idara, hususan idara ya huduma kwa taifa nchini, NYS sharti ziwekwe kwenye wizara ya elimu ili kuwalipa walimu kuliko serikali kushuhudia visa vya ufisadi ambavyo vinahusisha idara tofauti tofauti.
Alisema kuwa anaelewa masaibu walimu hao wanapitia kwani walimu wamedhulumiwa kwa muda mrefu, na ni wakati sasa masaibu yao kutupwa katika kaburi la sahau na kuanza maisha kama wafanyakazi wengine wa idara nyingine za serikali.
Baadhi ya wabunge ambao waliunga mkono usemi huo ni pamoja na Richard Onyonka, Ben Momanyi, na Manson Oyongo.