Familia ya kijana aliyeuawa na polisi mjini Mombasa imesisitiza kwamba watafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba aliyetekeleza mauaji hayo anachukuliwa hatua za kisheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Magaston Kenga, babake marehemu pamoja na mamake Ruth Syombua, wamesema kwamba mwanao, Tony Katana, aliyekuwa na umri wa miaka 16, hakuwa na uhusiano wowote na makundi ya uhalifu.

Wakizungumza siku ya Jumanne baada ya kuzuru kituo cha polisi cha Nyali walipokutana na OCS wa kituo hicho, wazazi hao walisema lazima maafisa waliomuua kijana wao afunguliwe mashtaka.

“Mimi nataka aliyetekeleza kitendo hicho afungwe jela. Siwezi kuwa na amani akiwa bado yuko mtaani,” alisema Bi Syombua.

Aidha, Syombua amesema tangu kitendo hicho kutokea, wamekuwa wakiishi kwa hofu bila kujua ni kipi kitakachotokea katika familia yao.

“Nahofia usalama wangu. Ata nimetoroka nyumbani kwangu kwa sababu sijui pengine watakuja kutumiminia risasi,” alisema Syombua.

Kwa upande wake, Bwana Kenga amesema kwamba mwanawe aliyekuwa katika kidato cha pili alikuwa tegemeo kubwa katika familia hiyo.

“Niko na majonzi sana. Nilikuwa namtegemea kijana wangu na sasa kile ninachotaka ni kuona mwanangu amezikwa na idara ya usalama iharakishe uchunguzi,” Bwana Kenga.

Tony Katana, mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Harvards mjini Mombasa, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi alipokuwa akitoka harusini.

Maafisa wa polisi katika kituo cha Nyali wamesema wanaendelea na uchunguzi kabla ya kuwasilisha ripoti kamili kwa mwendeshaji mkuu wa mashataka nchini.