Viongozi wa makanisa nchini wamesema wana imani kuwa Tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini IEBC, itaandaa uchaguzi huru na wa amani mwaka ujao.
Wakizungumza kwenye mkutano na makamishna wa IEBC jijini Nairobi siku ya Jumatanp, viongozi hao walisema kuwa hawaungi mkono maandamano ya mrengo wa Cord ya kushinikiza kubanduliwa kwa IEBC.
Viongozi hao waliutaka mrengo wa Cord kutafuta njia mbadala ya kusuluhisha mizozo baina yao na tume hiyo.
Katibu mkuu wa Baraza la kitaifa la makanisa nchini, Askofu Peter Karanja, alisema kuwa baraza hilo limedhihirisha kuwa tume hiyo imejitayarisha vilivyo kwa uchaguzi wa mwaka ujao.
Hata hivyo, mwenyekiti wa baraza hilo tawi la Mombasa Sheikh Muhdhar Khitamy, alisema kuwa kama viongozi wa kidini, hawajapata barua rasmi kutoka kwa pande zote husika kuhusiana na kuwataka viongozi wa kidini kuongoza maridhiano hayo.
Khitamy alisema kuwa kama viongozi wa kidini ,wako tayari kuwashirikisha washikadau wote wakiwemo viongozi wa vijana katika mazungumzo hayo.
“Tutawajumuisha wadau wote katika kutatua mgogoro huu kwani Kenya sio nchi ya viongozi wa kisiasa pekee bali ni la Wakenya wote kwa jumla,” alisema Khitamy.
Aidha, Khitamy alikanusha madai kuwa viongozi wa kidini tayari wameonyesha kuegemea upande mmoja.
Alisema kuwa wao kama viongozi wa kidini wanataka pande zote husika kukaa chini na kuzungumza.