Ukiona mji wa Kisii umengara na kupendeza jua kwamba kuna wale wanaovumilia kibaridi cha asubuhi kuhakikisha kuwa wenyeji na wageni wanapunga upepo mwanana.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafanya bidii ya mchwa, lakini changamoto wanazopitia si haba, zingine ni za kuhatarisha maisha yao kiafya.

Leo hii Hivisasa imekutana na mmoja kati ya wale wanaofanya usafi katika mji wa Kisii akiwa katika harakati za kupalilia maua.

Bwana huyo anasimulia masahibu na magumu wanayokumbana nayo katika kazi hii ya kujipatia riziki.

“kazi hii tunaifanya kila asubuhi, lakini ukiangalia kama mimi hapa sina kinga ya mikono (gloves), tulipewa lakini zimezeeka na ukienda kuuliza inachukua hata miezi tatu ili kupewa zingine," alisema Charles choti.

"Tunashika uchafu wa kila aina na huu ni mji mkubwa sana hata wengine gambuti (gumboots) zimeisha kabisa hapa kwa kisigino zimeraruka kabisa na tunakanyaga majitaka (sewage). Inafaa zikizeeka unarudisha unapewa zingine papo hapo ili na tusipate maradhi," alisimulia Choti.

“Tuko na watoto shuleni na hata niko mpaka na wajukuu wanaonitegemea, mshahara tunaopata ni kidogo hata hautoshi. Gavana mwenyewe hajawahi kututembelea hapa aone yale matatizo tunayopitia," alilalama Choti.

"Ni mwaka mmoja sasa tangu nianze kufanya hii kazi lakini sijawahi mwona akitutembelea. Tunamwomba angalau na sisi atutembelee tukiwa kazini aone vile tunateseka," aliongeza kusema.

Sasa wafanya kazi hao wanatoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kisii, au idara husika kuwapa kinga ya mikono na miguu ili kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari yanayotokana na majitaka.