Wazee wa muungano wa Maumau kutoka maeneo mbalimbali wameitaka serikali kuingilia kati na kuwasaidia kujumuisha wazee wote waliopigania.
Wakiongozwa na naibu katibu wa muungano huo Evanson Kangethe Mukunu kwa niaba ya viongozi wengine, viongozi hao kutoka Laikipia, Kuresoi, Molo na Nyeri wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwakumbuka na kuwapa mashamba.
Wazee hao wanasema wameumia na kuhangaika kwa kuishi maisha duni hata baada ya kile wanataja kuwa kukomboa Taifa la Kenya kutoka kwa ukoloni.
Aidha, wamemtaka rais Kenyatta kuwasaidia ili zoezi la fidia kwao liweze kuharakishwa na kuwafaa wengi wao ambao hali zao za maisha ni duni
Wazee hao walifika katika afisi kuu za chama cha TNA katika tawi la Nakuru kwa lengo la kumtuma mwenyekiti wa chama hicho kuwaombea fursa ya kufanya kikao na rais na kumshauri kama wazee.
Wameshutumu upinzani kwa kile wamesema kuwa ni kutokuwa na heshima kwa rais hususan katika matamshi yao hasaa wakati wa vikao vyao na hivyo kutaka wachukuliwe hatua mwafaka.
Kuhusu hela za wakongwe, wazee hao wametaja ubaguzi katika zoezi hilo wakisema kuwa idadi ya wanaofaidika ni ndogo,wakidai kuwa wanaonufaika ni wale wenye uhusiano mwema na machifu.