Kanisa la katoliki pamoja na waumini wa dhehebu hilo kutoka Kaunti ya Mombasa wamejiweka tayari kumpokea Papa Francis, ambaye anaingia nchini hii leo, Jumatano.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu jijini Mombasa kwenye makao makuu ya kanisa hilo, askofu mkuu wa jimbo la Pwani wa kanisa hilo Martin Kivuva alisema kuwa tayari washirika wote pamoja na viongozi wa kanisa hilo wameweka mikakati madhubuti kuona kuwa Papa Francis anafurahia mandhari ya nchi ya Kenya.
Aliwataka wakazi wote, hasa wale ambao watasafiri kutoka jimbo la Mombasa kelekea jijini Nairobi kwa mapokezi rasmi, kuendelea kuhubiri amani na umoja kwa watu wote si tu waumini wa dini ya kikatoliki, bali kwa kila mja ambaye ana nia na azimio la kuokolewa kiroho.
Kivuva alisisitiza umuhimu wa kuanza kuonyesha unyenyekevu na kujaribu kuiga Papa Francis ambaye amekuwa na hulka ya kuwajali watu ambao hawajiwezi katika jamii.
Aidha, aliwataka viongozi wa siasa kubadili mienendo yao, na kuanza kuongoza nchi katika maadili na misimamo ya kidini badala ya kuzidi kuhubiri chuki na ukabila miongoni mwa wakenya maskini, hali ambayo inaweza kuitumbukiza nchi kwenye ghasia kama ghasia za baada ya kura za mwaka wa 2007.