Siasa ni mchezo ambao walala hai hutumia kunyanyasa walala hoi.
Uhayawani huu uliopitwa na wakati unaendelezwa kwa kuhakikisha kwamba Wakenya tumechukiana kwa misingi mbalimbali.
Ubaguzi kazini, ugavi duni wa raslimali ya umma, vyama vya kisiasa na ukabila ni baadhi ya silaa wanazotumia wasiasa.
Mababu hawakukosea waliposema, vita vya panzi ni fuhara kwa kunguru.
Wengi wa wanasiasa huhakikisha kuwa wapiga kura wamebaki katika bahari ya umasikini ili waendelee kuwaomba siku nenda siku rudi.
Wao hujitajirisha hadi wana uwezo wa kusafiri kwa ndege wakati mlinzi wake hamudu kulipa nauli ya kurudi kwake baada ya kazi.
Wanakunywa na kula bila kujali Wakenya wengi walalao njaa kaskazini mashariki mwa nchi.
Magari yetu yanaharibiwa na barabara mbovu ilhali yao yanapanda milima na mabonde bila tashwishwi yoyote.
Wakati unahofia usalama wako kutoka kwa adui usiomjua, wao wanakabiliana na maadui wa kujitakia.
Mbona umbague Mkenya mwenzako kwa misingi ya kikabila?
Iwe imeaminika kwamba wao hula sana, ni wezi, wana maringo, hukasirika haraka, hawalindi ndoa, wana ushamba na mengineyo; jua kuwa hii ni imani inayohitajika kung’olewa akilini mwetu.
Tufouti ambazo zipo kutokana na kabila la mtu ndizo zinafanya Kenya kuwa nchi ya kipekee. Wenye nguvu tumeona wakituwakilisha katika kandanda na raga.
Kwa upande mwingine, wanaojua kukimbia wamefanya kila mtu ajue Kenya ni boma la talanta.
Tafadhali tuenzi tofauti zetu ili tujenge Kenya na tusifuate matamshi ya kijinga ya wanasiasa.