Serikali ya kaunti ya Nakuru imetakiwa kupeleka dawa kwenye vituo vya afya vilivyo katika wadi ya Solai kaunti ndogo ya Rongai, la sivyo wakaazi watafanya maandamano kulalamikia hali hiyo.
Wakaazi wa Majani Mingi na Banita wakizungumza na mwandishi huyu Jumanne, walisema ikiwa serikali haitasikiza kilio chao watalazimika kufanya maandamano hadi mjini Nakuru katika muda wa Juma moja lijalo kulazimisha serikali hiyo ya kaunti kuajibika.
Mmoja wa wakaazi hao kwa jina Josiah Kemboi alisema kwamba wameteseka kwa muda wa miezi mitatu ambapo vituo vya afya kwenye eneo hilo vimekosa dawa.
“Kila mara unapoenda hospitalini, unaambiwa ukanunue dawa kwa sababu hakuna, na tunasikia vituo vingine serikali ya kaunti ikitoa dawa,” alisema Kemboi.
James Koech akasema: "Ni kama tumesahaulika na viongozi wetu. Hapa maradhi ya kuumwa na tumbo hayaishi kwa sababu hatuna maji safi ya kunywa.”
Afisa mkuu wa afya Rongai Stephen Belion, amekiri hospitali za eneo hilo zinakumbwa na uhaba wa dawa, akisema dawa hizo zilifaa kufika kwenye kabla ya tarehe Feb 20, 2016.
“Huko Lengenet, Rongai na Moricho pia kuna uhaba huo, nani wito wetu kwamba wahusika waharakishe kutatua tatizo lililopo, ili kuzuia taharuki miongoni mwa raia,” alisema bwana Belion.
Hata hivyo MCA wa wadi ya Sowin Simon Molok alisema kwamba serikali ya kaunti ya Nakuru inakumbwa na matatizo ambayo hakufichua ni yapi, lakini mikakati imewekwa ili kuhakikisha hospitali hizo zimepata dawa haraka iwezekanavyo.