Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya afya ya umma katika kaunti ya Nakuru imeelezea matumaini kuwa itahitimisha lengo la idadi ya watoto watakaopewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio licha ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Msimamizi mkuu wa maswala ya afya katika kaunti hiyo Samuel King’ori amesema kuwa huku Jumanne ikiwa siku ya nne ya chanjo hiyo, shughuli hiyo imeendeshwa bila ya tashwishi yoyote na kuongeza kuwa walikuwa wakiwalenga watoto 394,687.

Kulingana naye, Kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki ilikuwa ikiongoza kwa asilimia 77 ya watoto waliopewa chanjo hiyo ikifuatiwa na eneo la Gilgil kwa asilimia 64.

Maeneo mengine ni kama vile Nakuru Kaskazini asilimia 61, Molo asilimi 58 huku eneo la Naivasha likiwa la mwisho na asilimia 57.

Mjini Naivasha, mvua kubwa inayoendelea kunyesha pamoja na ukosefu wa miundo msingi bora umefanya shughuli hiyo kuwa ngumu kulingana na King’ori.

Naye mkuu msimamizi wa maswala ya afya wilayani humo Oren Ombiro amesema kuwa maeneo ya Kirima, Kwa Wangu, Maella na Kongoni hayakuwa yakipitika kutokana na barabara mbovu.