Baraza la mawaziri wa kaunti nchini limezidi kuishtumu tume ya mishahara na marupurupu nchini kutokana na jinsi inavyotatua maswala ya mawaziri hao.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo Antony Njaramba, waziri hao walisema kwamba iwapo maswala yao hayatatatuliwa kwa mjibu wa katiba ya nchi, basi watawaishtaki tume hiyo pamoja na makamishna kwa kushindwa kutatua changamoto wanazopitia.
Katika mahojiano na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Njaramba alisema kwamba tume hiyo imeshindwa kueleza bayana usawa wa viwango vya kazi na jinsi wanavyostahili kulipwa kwani wengi wa mawaziri hao hawajapata marupurupu ya kazi kwa muda mrefu licha ya kupitia changamoto nyingi mashinani.
"Tunaitaka tume ya SRC kujitokeza waziwazi na kueleza kinachoendelea katika tume hiyo kwani wengi wa mawaziri wa kaunti hukosa kupata marupurupu yao ya kikazi na wanapitia changamoto nyingi sana mashinani kumtekelezea mkazi miradi ya kimaendeleo, na iwapo watazidi kukaidi shinikizo letu, basi tutaishtaki tume hiyo pamoja na makamishna wao mahakamani," alisema Njaramba.
Njaramba ameshikilia kwamba sharti tume hiyo iandae vikao vya mazungumzo na viongozi wa baraza hilo na kujadili utata uliyopo ili kusitisha mgogoro unaowakumba mawaziri hao wa kaunti kwa muda wa zaidi ya miaka miwili.
Awali, tume ya SRC ilisema kwamba ugatuzi haujawaangazia vyema jinsi mawaziri hao wanavyofaa kulipwa marupurupu yao na swala hilo linashughulikiwa.
Haya yalijiri baada ya mawaziri hao wa kaunti kudai kuwa tume ya SRC imekosa kuwaangazia vyema katika maswala ya marupurupu kulingana na viwango vyao vya kikazi na licha ya shughuli ngumu wanazopitia mashinani.