Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki amesema bunge la kaunti hiyo litahakikisha limepitisha miswada muhimu ya kufanikisha maendeleo kwa wakaazi wa kaunti hiyo.
Ondieki alisema kaunti ya Kisii iko tayari kuleta maendeleo kwa wakaazi na kuna haja kwa bunge la kaunti hiyo kujumuika pamoja kuleta maendeleo haswa kupitia miswada bungeni.
Akizungumza mjini Kisii Ondieki alisema yeye kama spika na wabunge wa kaunti hiyo wanaunga mkono maendeleo kwani walichaguliwa kufaidi wakaazi.
“Tutahakikisha maendeleo mengi yameletwa katika kaunti yetu kupitia miswada muhimu ili tujenge kaunti yetu,” alisema Ondieki.
Aidha, naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi naye aliomba wakaazi wa kaunti hiyo kushirikiana na viongozi wa kaunti kufanya maendeleo mengi zaidi.
Maangi alisema wanahitaji kaunti ya Kisii kupiga hatua kwa mendeleo haswa katika ukarabati wa barabara, miradi ya maji, kufanikisha elimu kupitia mgao wa basari na mengine mengi ambayo yatanufaisha wakaazi.