Mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti ya Kisii Wilfred Chepkawai amejitolea kuona kwamba shule za msingi na za upili katika kaunti hiyo zinapata makocha wa riadha waliofuzu ili kuwafaa wanafunzi walio na talanta shuleni.
Chepkawai alikuwa akiongea katika Bewa Kuu la Chuo Kikuu cha Kisii Jumamosi baada ya kukamilika mashindano ya riadha miongoni mwa shule za upili kutoka kaunti ya Kisii, alisema kuwa wanafunzi wa shule za eneo hilo wana uwezo wa kunyakua ubingwa hata wa kimataifa ila wamekosa makocha walio na utaalam wa kimataifa.
Alishangaa ni kwa nini jamii ya wakisii ambayo ilmewahi kuwa ya kwanza Kenya kuleta medali ya dhahabu imedidimia kwenye nyanja za riadha huku akiwapa changamoto ya kuwa na ushirikiano na wanariadha kutoka sehemu hiyo na kutembelea ofisi yake kupata ushauri pamoja na habari zinazohusu michezo na elimu kwa jumla.
"Kisii ina uwezo mkubwa wa kushindana na wanariadha wa kimataifa; kama una talanta kuwa huru kuwasiliana na mimi au afisi yetu ili kupata msaada unaohitajika," Chepkawai alishauri.
Mkurugenzi huyo ambaye pia ni mwanakamati wa michezo alichukua nafasi hiyo kuwatambulisha makocha 6 wa riadha wa kimataifa kutoka sehemu ya Kisii ambapo aliahidi kuwashawishi Kaunti ya Kisii kuwatambulisha kwa Gavana James Ongwae kwa kuwapa nafasi kutoa ujuzi wao kwa vijana wenye talanta.