Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kisumu Mashariki Moses Ole Tutui, amewahakikishia wakaazi wa Kisumu na viunga vyake usalama wa kutosha msimu huu wa sherehe za krisimasi na mwaka mpya.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Kisumu siku ya Alhamisi, Ole Tutui alisema kuwa maafisa wa utawala waliokuwa likizoni wamelazimika kurejea kazini, ili kuimarisha usalama katika maeneo yao ya kazi.
“Ningependa kuwahakikishia wananachi wa Kisumu usalama wa kutosha kipindi chote cha sherehe za Krisimasi na mwaka mpya. Wasiwe na hofu yoyote ila wana jukumu la kupiga ripoti kwa polisi, iwapo watahisi kwamba kuna kisa chochote cha kutatiza usalama na amani,” alisema Ole Tutui.
Aliongeza kuwa maafisa wa polisi wa kawaida na wale wa utawala, wanaendelea kushika doria katika maeneo yote ya kaunti ya Kisumu, pamoja na kuandaa msako dhidi ya wahalifu.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa makanisa yatakayoandaa kesha, kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha.