Wanabodaboda kutoka eneo la Kiogoro, eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii wameiomba serikali ya kaunti ya Kisii kuwajengea vibanda vya kuegesha bodaboda zao katika eneo hilo hasa wakati wa jua na wa mvua.
Wakiongea siku ya Jumatano katika eneo la Kiogoro wakiongozwa na mwenyekiti wao Daniel David pamoja na mfanyibiashara bw Job Nyatundo, wanabodaboda hao wamesema kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka kwa jua na pia wakati wa mvua kwa sababu ya ukosefu wa vibanda hivyo ambavyo angalau vitatumika kusubiri wateja wao jambo ambalo huwalazimu kujikinga mbele ya duka za watu.
“Kwa muda sana tumekua tukiteseka licha ya serikali ya kaunti ya Kisii kusema kuwa kuna mpango wa kujenga vibanda hivyo lakini ajabu ni kuwa bado tunateseka lakini bado hatujakufa moyo tunaomba serikali kusikia kilio chetu na kutujtengea vibanda hivyo,” alisema David.
Aidha, David alisema kwamba wanaendelea kupoteza wateja wao na biashara yao inaendelea kurudi chini kwa sababu ya hali mbaya ya barabara za eneo bunge la Nyaribari Chache ambazo hazipitiki hasa wakati huu wa mvua na hivyo kumuomba mbunge wa eneo hilo Richard Tong’i kuwakarabatia barabara hizo kwa ushirikiano na kaunti ya Kisii.