Unywaji wa pombe katika Kaunti ya Kiambu inasemekana kuwa mojawapo ya changizo ya dhaluma za kinyumbani na ambalo ni janga kubwa la kibinadamu kote nchini.
Katika mahojiano na baadhi ya wanawake katika soko la Kiambu, darubini iliweza kutambua kuwa wanaume wengi wamebadili vilabu na kuvifanya makaazi yao huku familia zao zikisaga meno wasipate cha kula wala cha kunywa.
Akionekana mwenye huzuni na aliyesongwa na mawazo, mkaazi wa eneo hilo Mercy Nyawira anasikitikia kufungwa jela kwa mumewe aliyetishia kuteketea nyumba yao na hapo kupatwa na mkono wa Serikali.
Nyawira alidokeza kuwa vita vya kila uchao ni mojawapo ya changamoto sugu alizokumbana nazo endapo baba watoto wake angerejea nyumbani akiwa amelewa chakari.
“Kwa mfano siogopi nikisema kwamba, bwanangu yumo gerezani kwa minajili ya ulevi, amani tuliyokuwa nayo hapo awali ilitoweka na sasa vita vinatawala pale nyumbani,” alisema Nyawira.
Unywaji wa tembo kupindukia na wanaume kutoka Kaunti hiyo umepelekea kuwafanya wake zao kuchukua sheria mikononi mwao na kuwadhuru waume zao kwa njia mbalimbali kwa kutoajibika kama vichwa wa familia.
Kwa mujibu wake Juliet Kwamboka ambaye ni msusi mjini Kiambu, iwapo wanaume na wanawake wataajibika katika majukumu yao ya kifamilia, visa vya mavamizi kama kuchomwa na maji moto, kung’olewa kwa sehemu nyeti na kukatwa na panga vitapungua.
Aidha Kwamboka alisisitiza kuwa kuepuka na filamu na nakala zinachangia dhuluma za kinyumbani ni mojawapo wa njia mwafaka za kukemea vurugu katika familia.
Masikitiko makubwa yake Stephen Muthee, Mhubiri katika Kanisa la Newlight International mjini Kiambu, ni kwa watoto wanaoshuhudia masaibu haya katika familia zao, akisema kuwa hawapati maadili mazuri ya jinsi ya kuzilinda familia zao za siku za usoni.
“Vijana wetu wanaanza kunywa vileo wakiwa na umri mchanga mno kufuatia yale wanayoyaona kwa wavyele wao wanapokuwa hivyo kuubomoa msingi wao mwema wa maisha,” Alisema Mhubiri Muthee.