Kupitia mitandao ya Facebook na WhatsApp, wakaazi wa kaunti ya Nakuru wadi ya Bahati wameilazimisha serikali ya kaunti yao kupitia wizara ya mali asli, mazingira, maji na kawi kuondoa takataka zilizokuwa zimerundika katikati ya soko la Bahati.
Jumanne watumizi wa mitandao waliweka picha za takataka hizo kwenye Facebook, wakihoji mbona amri ya gavana Kinuthia Mbugua mwishoni wa mwezi October imeendelea kupuuziliwa na mawaziri wake.
Ujumbe ulioandikwa kwenye Facebook Jumanne tarehe 17 mwezi huu ulisema; “Wakati gavana Kinuthia Mbugua alitembelea wadi ya Bahati tarehe 22 mwezi Oktoba mwaka huu, alitoa amri kwamba jaa hili la takataka liondolewe akihofia lingebatizwa jina lake, ambapo aliwaamrisha mawaziri wa mazingira na fedha kuhakikisha limeondolewa mara moja.”
Ujumbe huo ukaendelea kusema,“Hata hivyo, wiki tatu baadaye, takataka hizo zingalipo, zikitoa uvundo mkali na kuhatarisha afya ya wenyeji,” ambapo walihoji kama hiyo inadhihirisha ukosefu wa utiifu kwa kiongozi wa kaunti.
Hata hivyo saa chache baadaye, tinga la kukusanya takataka lilitumwa kwenye soko hilo, na kuuondoa uchafu huo.
Mwakilishi wa wadi hiyo katika bunge la kaunti ya Nakuru Peter Nderitu, alisema juhudi za kuwasiliana na waziri husika zilikuwa zimeshindikana, ila hangeweza kudhibitisha kama jumbe na picha hizo za mitandao ni kati ya zilizofanya maafisa husika kuwajibika.
“Ni kweli sasa takataka hizo zimeondolewa, huenda walisoma jumbe hizo au walipata habari kwa njia zingine,” alisema Nderitu.