Askofu wa Kanisa la Deliverance Dr Mark Kariuki amekashifu vikali dhana ya Wakenya kuwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017 utakumbwa na ghasia mbaya zaidi kuliko zile ambazo zilishuhudiwa mwaka wa 2007.
Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa ujenzi wa hoteli ya kifahari ambayo itajengwa kwa ushirikiano baina ya kanisa hilo na Heri Home huko Nyali, Mombasa, Askofu Kariuki alisema kuwa viongozi wengi pamoja na wagombea viti tofauti wamekuwa wakitabiri ghasia.
Kariuki alisema kuwa kama kiongozi wa dini, hataruhusu hayo kutendeka.
Alisema kuwa hata viongozi ambao wanategemea nguvu za giza kutoka kwa waganga hawatafanikiwa, kwani wao ndio huchangia pakubwa katika kuhujumu juhudi za amani nchini.
Kiongozi huyo wa dini pia amewashauri wakaazi wa Mombasa na Wakenya kwa jumla kuwekeza katika biashara mbalimbali, ili waweze kujikimu na kujiimarisha kimaisha.