Share news tips with us here at Hivisasa

Uchaguzi wa chama cha ODM katika Kaunti ya Nyamira umefutiliwa mbali.

Kulingana na mshirikishi wa zoezi hilo Peter Odoyo, uchaguzi huo haukufanyika kwa njia halali baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, Alfred Ndubi, kutiwa mbaroni na maafisa wa polisi wa Kituo cha Nyamira, kwa madai yakuwachochea wajumbe wa chama hicho kuzua vurugu.

"Tumeamua kufutilia mbali uchaguzi wa chama cha ODM Nyamira kwa kuwa ulikumbwa na utata baada ya msimamizi aliye stahili kusimamia uchaguzi huo kutiwa mbaroni kwa madai yakuwachochea wajumbe," alisema Odoyo.

Akizungumza na mwandishi huyu katika mahojiano kwa njia ya simu siku ya Alhamisi, Odoyo alisema uchaguzi huo haukuzingatia suala la usawa wa kijinsia kwa kuwa idadi kubwa ya waliochaguliwa walikuwa wanaume.

"Uchaguzi huo aidha haukuzingatia usawa wa kijinsia kwa kuwa wanaume wengi walichaguliwa, ikilinganishwa na idadi ya wanawake," alisema Odoyo.

Odoyo alisema kuwa sasa itawalazimu maafisa wasimamizi wa uchaguzi huo kutenga tarehe nyingine ya kurudia zoezi hilo la uchaguzi.