Mkurugenzi mkuu wa shirika la Haki Africa Hussein Khalid akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Uchaguzi wa marudio ya urais haukuwa wa uwazi na haki ingawa ulikuwa huru na wa amani.Haya ni kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika.Shirika hilo limebaini kuwa uchaguzi huo haukuafikia vigezo hitajika wakati wa kuandaliwa kwake.Akizungumza na wanahabari wakati wa kuzindua ripoti yao ya uangalizi kuhusu uchaguzi huo siku ya Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa Haki Africa Hussein Khalid alisema hakukuwa na mawakala wakuthibithisha iwapo masunduku ya kupigia kura yalikuwa sawa, na iwapo fomu 34A zilikuwa hazijajazwa.“Mawakala wa wagombea wengine hawakuwa vituoni hivyo basi hakukuwa na uwazi wowote,” alisema Khalid.Aidha, Khalid alisema kuwa idadi ya watu walioshiriki uchaguzi huo ilishuka kwa asilimia 70 ikilinganishwa na uchaguzi wa Agosti 8, huku wagombea wote wakipata idadi ndogo ya kura ikilinganishwa na uchaguzi wa Agosti.“Uchaguzi huu wa marudio ulishuka pakubwa ikilinganishwa na ule wa Agosti nane,” alisema Khalid.Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo, kura alizopata Rais mteule Uhuru Kenyatta zilishuka kwa asilimia 21.3 ikilinganishwa na kura alizopata mwezi Agosti, huku Ekuru Aukot akishuka kwa asilimia 49.9 ikilinganishwa na kura alizopata awali.Uhuru aliibuka mshindi katika uchaguzi huo baada ya kupata kura 7,483,895 naye Raila Odinga akipata kura 73,228 licha ya kususia uchaguzi huo.Mohammed Abduba Dida alijizolea kura 14,107, Japhet Kavinga kura 8,261, huku Micheal Wainaina akipata kura 6,007.Joseph Nyagah alipata kura 5,554, Ekuru Aukoth wa chama cha Thirdway Alliance akiwa na kura 21,333 naye Cyrus Jirongo wa chama cha UDP akiwa na kura 3,832.