Wakuu wa polisi mjini Mombasa pamoja na wakuu wa ujasusi wanatarajiwa kuzuru eneo la Shonda huko Likoni, ambako kijana mmoja anadaiwa kupigwa risasi na afisa wa polisi kimaksudi.
Katika ziara yake katika eneo la Likoni siku ya Alhamisi, Mkuu wa polisi katika kanda ya Pwani Francis Wanjohi alisema kuwa uchunguzi dhidi ya kisa hicho lazima uanzishwe mara moja ili ukweli ubainike.
Wanjohi pia alitoa wito kwa wakaazi wa eneo hilo ambao wana ushahidi wowote kuwasilisha ujumbe kwa maafisa wa polisi.
Familia ya kijana huyo ilidai kuwa mwanao alipigwa risasi na afisa wa polisi anayehudumu katika eneo la LIkoni walipokuwa wakishika doria.
Familia hiyo aidha ilidai kuwa afisa huyo alikuwa na nia ya kumuua kijana huyo.
Hata hivyo, Naibu mkuu wa polisi wilayani Likoni Anthony Shimoli alikana shtaka hilo na kuwatetea maafisa hao wa polisi.
Shimoli aliwataka walio na ushahidi kuhusu madai hayo kuandikisha taarifa kwa polisi.