Maafisa wa polisi mjini Mombasa wanaendeleza msako kuhusiana na genge lililovamia jumba la Habo Agencies linalomilikiwa na Mbunge wa Nyali Hezron Awiti na kuharibu mali.
Kulingana na maafisa hao, genge hilo ambalo nia yake haijabainika lilivamia jumba hilo siku ya Ijumaa na kuvunja vioo, pamoja na kuharibu mali yenye thamani ya mamilioni ya pesa.
Afisa mkuu wa Idara ya upelelezi katika Kaunti ya Mombasa Jacob Kanake amesema kwamba hadi sasa bado hawajamtia nguvuni mshukiwa yeyote kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo, alisema kuwa wamekusanya habari muhimu zitakazopelekea kunaswa kwa majambazi hao.
Awiti aliwakosoa maafisa wa polisi kwa kusema kuwa licha ya yeye na familia yake kuvamiwa mara kadhaa, maafisa hao hawajafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na msururu huo wa visa vya uhalifu vinavyomuandama.