Afisa wa Afya katika Kaunti ya Kisumu Arthur Shikanda amesema kuwa ni hatia kupikwa na kuuzwa kwa vyakula vilivyopikwa bila kuzingatia usafi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Shikanda alisema kuwa huenda kukatokea mkurupuko wa ugonjwa wa kipindu pindu almaarufu cholera katika Kaunti hiyo iwapo wachuuzi wataendelea kupika na kuuza vyakula kwenye mazingira chafu.

Kwenye mahojiano Mwandishi wa Habari huyu jijini Kisumu siku ya Jumatano, Shikanda alisema kuwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakichuuza chakula kiholela jijini Kisumu wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka katika juhudi za kuzuia mkurupuko wa kipindu pindu Kisumu.

“Hatutaki kuona chakula ambacho kinauzwa reja reja, hakijulikani kimepikiwa wapi na kwa mazingira yapi. Lazima tujue chakula kimepikiwa wapi kabla ya kuruhusu kiuzwe mitaani,” alionya Shikanda.

Hata hivyo, baadhi ya wachuuzi wa chakula jijini Kisumu tuliozungumza nao wamepuuzulia mbali agizo la Serikali ya Kaunti ya Kisumu kupiga marufuku uchuuzi wa chakula huku wakiishtumu Idara husika kwa utepetevu katika kudumisha usafi.

Wachuuzi hao wamesema kuwa maafisa husika, wana jukumu la kuhakikisha kuwa usafi unazingatiwa kote, kama njia moja ya kuzuia kuzuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu katika Kaunti ya Kisumu.

“Ugonjwa wa kipindu pindu hautokani tu na kuuza chakula kando ya barabara, bora tu kimepikwa kwenye mazingira masafi. Usafi wa maeneo yote ya jiji la Kisumu na viunga vyake ni muhimu sana kwa hivyo Serikali ya Kaunti inafaa kufanya usafi katika mji wetu,” alidai mmoja wa wachuuzi katika mji huo wa Kisumu.